Pata taarifa kuu
GAMBIA-SIASA

Adama Barrow ashinda urais nchini Gambia, Rais Jammeh akubali kushindwa

Adama Barrow ametangazwa kuwa mshindi wa Uchaguzi wa urais nchini Gambia baada ya kumshinda rais Yahya Jammeh ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo kwa miaka 22.

Adama Barrow, mshindi wa Uchaguzi wa urais nchini Gambia
Adama Barrow, mshindi wa Uchaguzi wa urais nchini Gambia STR / AFP
Matangazo ya kibiashara

Tume ya Uchaguzi nchini humo, imesema baada ya kura kuhesabiwa, rais Jammeh alikubali kuwa mpinzani wake  Barrow, aliyewakilisha vyama vya upinzani katika Uchaguzi huo amemshinda.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini humo Alieu Momar Njie, amewaambia wanahabari jijini Banjul kuwa Barrow alipata ushindi baada ya kupata kura 263,515 huku rais Yahya Jammeh akiwa wa pili kwa kupata kura 202,099.

Njie amesema imewashangaza wengi baada ya rais Jammeh kukubali matokeo.

“Hakika ni ajabu sana kwa mtu ambaye amekuwa akiongoza nchi hii kwa muda mrefu kukubali kushindwa,” amesema jijini Banjul.

Ushindi wa upinzani umepokelewa kwa furaha kubwa sana nchini humo hasa jijini Banjul, eneo ambalo limekuwa ngome kubwa ya rais Jammeh kwa muda mrefu.

 

Rais  Yaya Jammeh
Rais Yaya Jammeh ISSOUF SANOGO / AFP

Wapiga kura wapatao 800,000 walipiga kura siku ya Alhamisi kumchagua rais katika taifa hilo dogo la Afrika Magharibi.

Kuelekea kwenye Uchaguzi huu, rais Jammeh alionya kuwa maandamano hayatakubalika nchini humo baada ya matokeo ya mwisho.

Barrow, akizungumza na RFI wiki hii, alisema kuwa alikuwa na matumaini makubwa ya kushinda uchaguzi huu ikiwa utakuwa huru na haki.

Kwa mara ya kwanza, vyama saba vya upinzani viliungana na kumteua Barrow ambaye ni Mfanyibiashara kuwania urais nchini humo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.