Pata taarifa kuu
BURUNDI-EU-MISAADA

Ni madhara yapi kwa Burundi baada ya EU kusimamisha misaada yake?

Umoja wa Ulaya (EU) umeamua Jumatatu hii Machi 14 kusimamisha misaada yake ya kifedha kwa nchi ya Burundi, miezi mitatu baada ya mashauriano kuhusu nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Alain Aimé Nyamitwe.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Alain Aimé Nyamitwe. RFI / Gaël Grilhot
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu umechukuliwa kulinagana na Ibara ya 96 ya Mkataba wa Cotonou ambao unasimamia ushirikiano kati ya mataifa ya Ulaya na Afrika.

Mwezi Desemba mwaka jana, Baraza la Umoja wa Ulaya lilibaini kwamba juhudi zinazofanywa na serikali ya Bujumbura kwa kurekebisha ukiukaji wa haki za binadamu na kanuni za demokrasia hazitochelezi. Uamuzi wa Umoja wa ulaya unaweza kuwa na madhara makubwa kwani uchumi wa nchi hiyo umefikia pabaya.

Baada ya Ubelgiji, Uholanzi na Marekani, ni zamu sasa ya Umoja wa Ulaya ya kusimamisha misaada yake ya moja kwa moja kwa utawala wa Burundi ikiwa ni pamoja na msaada wa bajeti. Umoja wa Ulaya ulikuwa mfadhili mkubwa kwa nchi ya Burundi na umekua ukichangia 20% ya bajeti ya taifa hilo.

Nchini Burundi, Wizara ya Kilimo na ile ya Afya zinapewa kila Wizara ruzuku kwa kiwango cha 80% na 60% kwa misaada kutoka nje ikimaanisha kwamba madhara yanaweza kuwa makubwa kwa raia ambao tayari wanakosa madawa, huku bei za vyakula zikiongeza siku kwa siku. Ni kwa sababu hii, Umoja wa Ulaya umeamua kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu na inapania kuendeleza miradi yenye faida ya moja kwa moja kwa raia bila kupitia kwenye akaunti za serikali.

Ili kurejesha misaada yake, Umoja wa Ulaya unasubiri serikali ya Bujumbura kuchukua "hatua madhubuti" kwa kuketi kwenye meza ya mazungumzo na upinzani, mazungumzo ambayo yamesimama tangu mwezi Desemba mwaka jana.

Nchini Burundi, mgogoro sio tu wa kisiasa lakini pia a kifedha. Katika suala la pato la ndani, Burundi leo ni nchi ya mwisho. Hazina za serikali ni tupu na utabiri wa Shirika la Fedha Dunia IMF kwa mwaka 2016 ni majanga tu. Hali ambayo inaonekana kutomtia wasiwasi Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Alain Aimé Nyamitwe.

"Tunajifunza kwamba tunapaswa kutegemea rasilimali zetu na misaada ya wafadhili wetu wengine," Alain Aimé Nyamitwe amesema, bila hata hivyo kufafanua wafadhili gani hao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.