Pata taarifa kuu
BURUNDI-UN-HAKI ZA BINADAMU

Wataalam wa UN kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu Burundi

Wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa wanohusika na kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa kwa kipindi cha miezi 10 ya mgogoro nchini Burundi watawasili mjini Bujumbura Jumanne hii. Taarifa hii imetolewa Jumatatu hii na afisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Kaburi la halaiki linalodaiwa kugunduliwa katika msitu wa Rukoko karibu makaburi ya Mpanda ambapo mashahidi wanasema waliona miili 15 ya askari na raia wakizikwa na askari polisi baada ya mashambulizi ya Desemba 11.
Kaburi la halaiki linalodaiwa kugunduliwa katika msitu wa Rukoko karibu makaburi ya Mpanda ambapo mashahidi wanasema waliona miili 15 ya askari na raia wakizikwa na askari polisi baada ya mashambulizi ya Desemba 11. RFI/Sonia Rolley
Matangazo ya kibiashara

Wataalam hao watatu, ambao Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa liliomba kutumwa nchini Burundi Desemba 17, wana dhamana ya "kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu na dhulma ili kuzuia kuzorota kwa hali ya mambo nchini Burundi."

"Lengo letu ni kuisaidia serikali (ya Burundi) kwa kutimiza majukumu yake juu ya haki za binadamu na sheria ishike mkondo wake kwa yeyote yule ambaye atakua amehusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na kutambua wahusika, " amesema Christof Heyns, raia kutoka Afrika Kusini, ambaye ni afisa maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya watu waliokua mikononi mwa vyombo vya dola.

"Tumepokea majukumu yalio wazi ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ili kuisaidia Burundi kuepukana na hali mbaya ambayo inaweza kutokea kwa wakati wowote," ameongeza Maya Sahli-Fadel, raia kutoka Algeria, ambaye ni afisa Maalum wa Umoja wa Afrika kuhusu wakimbizi, watu wanaoomba hifadhi, wakimbizi wa ndani na wahamiaji barani Afrika.

Watatu miongoni mwa wataalam hao ni raia kutoka Colombia, Pablo de Greiff, afisa maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uendelezaji wa ukweli, sheria, fidia na dhamana isiyo ya marudio.

"Kutumwa kwa ujumbe huu haikuwa rahisi kwa sababu serikali ya Burundi kwanza iliongeza vikwazo (...) Hali hii ilitengamaa wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi wiki moja iliyopita ", afisa wa Umoja wa Mataifa, ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameliambia shirika la habari la Ufaransa la AFP.

Ujumbe huo utakaoendesha uchunguzi utawasilisha ripoti yake ya awali Machi 21 na ripoti yake ya mwisho mwezi Septemba.

Hayo ya kijiri miili ya watu watatu imegunduliwa katika kaburi la pamoja Jumatatu wiki hii katika kata ya Mutakura wilayani Cibitoke, kaskazini magharibi mwa jiji la Bujumbura, Meya wa mji huo mkuu wa Burundi, Freddy Mbonimpa, ameliambia shirika la habri la Ufaransa la AFP.

Wakati huo huo shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la FIDH linasema kuwa hatua ya serikali ya burundi kuanzisha sensa ya wageni nchini humo ni njama ya kutaka kuminya uhuru wa waandishi wa habari na wote ambao wanaweza kutoa ushuhuda wao kwa kile kilichotokea.

Burundi imetumbukia katika machafuko ya kisiasa kwa miezi 10 sasa, kutokana na nia ya Rais Pierre Nkurunziza kutaka kusalia madarakani kwa muhula wa tatu, ambao aliupata mwezi Julai, baada ya kuchaguliwa, uchaguzi ambao ulisusiwa na vyama vikuu vya upinzani, hata jumuiya ya kimataifa ilikataa kuhudhuria uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa upinzani, vyama vya kiraia na baadhi ya wafuasi vigogo wa chama madarakani CNDD-FDD, uchaguzi wa Rais Nkurunziza unakiuka Katiba na Mkataba wa Amani na Maridhiano wa Arusha uliokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1993 na 2006, ambapo watu 300,000 waliuawa.

Machafuko yanayoendelea nchini Burundi yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 400 na kusababisha watu zaidi ya 240,000 kukimbilia nje ya nchi. Mashirika ya haki za binadamu yamekua yakibaini kuwepo kwa makaburi ya halaiki, matukio mengi ya mauaji ya watu ambao walikua mikononi mwa vyombo vya dola na mauaji ya kuvizia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.