Mawakili wa Gbagbo, wasema rais Ouattara aliingia madarakani kwa kutumia nguvu akisaidiwa na Ufaransa
Mawakili wa utetezi wa rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, wanamtuhumu rais wa sasa, Alassane Ouattara kwa kuchukua madaraka kwa nguvu akisaidiwa na taifa la magharibi lililowahi kuitawala nchi hiyo, Ufaransa.
Imechapishwa:
Katika maelezo yao ya awali kwenye mahakama ya ICC ikiwa ni siku ya tatu toka kuanza kwa kesi dhidi ya kiongozi huyo, ambapo wakili wake, Emmanuel Altit ameileza mahakama namna ambavyo Ufaransa ilimsaidia Ouattara kuchukua madaraka kwa nguvu.
Wakili Altit, ameongeza kuwa, rais Ouattara na wafuasi wake, walitaka kuchukua madaraka kwa nguvu ikiwa ni pamoja na kugombea mji wa Abidjan, ilikuwa ni wazi kabisa kuwa mpango wake ulipangwa kwa kusaidiwa na Ufaransa.
Gbagbo na mtuhumiwa mwingine, Charles Ble Goude, kiongozi wa kundi la vijana lililokuwa linamuunga mkono, wamekana mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu baada ya watu elfu 3 kuuawa wakati wa vurugu za mara baada ya uchaguzi mkuu wa 2010.
Kesi hii ya aina yake ambayo ni ya kwanza kushuhudia rais wa zamani akisimama kizimbani, inatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka mitatu.
Gbagbo alijitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi wa mwaka 2010, lakini mataifa yenye nguvu duniani ikiwemo Marekani na Ufaransa pamoja na umoja wa Mataifa walimuunga mkono Ouattara aliyeshinda kwa idadi ndogo ya kura.
Mawakili wa Gbagbo wamewaambia majaji wa mahakama ya ICC, kuwamteja wao ametengenezewa kesi, kesi ambayo wahusika wake ni taifa la Ufaransa, ambalo lilihakikisha Ouattara anaingia madarakani kwa nguvu.