Pata taarifa kuu
BURUNDI-HRW-UCHUNGUZI

Burundi: HRW yaomba uchunguzi huru haraka iwezekanavyo

Nchini Burundi, siku moja baada ya zaidi ya maiti 70 kuokotwa zikitapakaa katika mitaa ya jiji la Bujumbura, vikosi vya usalama na ulinzi vinatuhumiwa kutekeleza mauaji hayo katika maeneo kulikoshuhudiwa maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa Pierre Nkuruniza.

Wakazi wakiangalia mwili wa mtu aliyeuawa katika wilaya ya Nyakabiga, Bujumbura, Desemba 12, 2015.
Wakazi wakiangalia mwili wa mtu aliyeuawa katika wilaya ya Nyakabiga, Bujumbura, Desemba 12, 2015. © REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana
Matangazo ya kibiashara

Kwa upande wao, viongozi wanajitetea wakisema kuwa waliwaua "maadui" zaidi ya 80. Shirika la Marekani la Haki za Binadamu la Human Right Watch (HRW) limeomba Jumapili hii Desemba 13, uchunguzi huru ufanyike.

Shirika hilo linaomba uchunguzi "sahihi ulio huru" uanzishwe haraka iwezekanavyo na kwamba "wataalam waweze kutoka nje" ili kusaidia wachunguzi wa Burundi.

"Haya ni mauaji makubwa kuwahi kutokea nchini Burundi tangu kuanza kwa mgogoro mwezi Aprili mwaka huu. Tunaomba uchunguzi sahihi ulio huru uanzishwe haraka iwezekanavyo. Kutokana na mambo ya kisiasa na rushwa ambavyo vinaukabili mfumo wa vyombo vya sheria nchini Burundi, wataalam wanapaswa kutoka nje", Carina Tertsakian, mtafiti katika shirika la haki za binadamu la Human Right Watch (HRW) ameiambia RFI.

Human Rights Watch imelaani kitendo cha polisi na viongozi wa maeneo kulikoshuhudiwa maiti hizo "kuharakia kuondoa maiti kabla ya kuendesha uchunguzi", huku wakizuia watu kusogelea maeneo hayo, kwa mujibu wa mashahidi. Mashahidi pia wanalaani ripoti iliyotolewa na jeshi ya watu 79 waliouawa wakati zaidi ya vijana 200 waliuawa katika maeneo ambayo ni kitovu cha maandamno dhidi ya muhula wa tatu wa Pierre Nkuruziza.

"Inaonekana kwamba jitihada za kuweka wazi kilichotokea zilivurugwa na polisi pamoja na viongozi wa maeneo kulikoshuhudiwa maiti hizo. Hapo tena, ni dhahiri kuwa inaonyesha ukosefu wa nia njema kutoka kwa viongozi kuhusiana na matukio hayo. Aidha,serikali ya Burundi, tangu kuanza kwa matukio hayo, imekua ikitoa taarifa za kutisha zinazotofautiana. Serikali imekua ikidai kuwa imedhibiti hali ya usalama, wakati ambapo kila kukicha kumekua kukiokotwa katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura miili ya watu waliouawa na, hivi sasa kumeshuhudiwa maiti nyingi zikitapakaa mitaani ", Carina Tertsakian ameelezea wasi wasi wake.

Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, ziliyokusanywa na Human Right Watch, ambazo bado hazijathibitishwa, idadi ya watu waliouawa imeongezeka na kufikia zaidi ya 100. Hii huenda ni idadi ya mashambulizi yalioendeshwa na waasi katika kambi za kijeshi kadhaa mjini Bujumbura na katika mkoa wa Bujumbura Ijumaa asubuhi, na vurugu ziliyofuata.

Tangu mapinduzi yaliyoshindwa mwezi Mei, yaliosababishwa na uamzi wa Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu, vurugu za hivi karibuni ni mbaya zaidi kutokea nchini Burundi. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, tangu kuanza kwa machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili, mamia ya watu waliuawa na zaidi ya watu 200, 000 walilazimika kukimbilia nje ya nchi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.