Pata taarifa kuu
BURUNDI-SIASA-USALAMA

Zaidi ya watu 4 wauawa Kaskazini mwa Burundi

Watu zaidi ya wanne wameuawa na wengine zaidi ya ishirini wamejeruhiwa katika mashambulizi ya guruneti dhidi ya baadhi ya baa za mikoa ya Kirundo, Ngozi na Kayanza, Kaskazini mwa Burundi.

Mwanajeshi akibebelea silaha ya kivita wakati wa maandamano ya raia wanaopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza, Bujumbura, Mei 15 mwaka 2015.
Mwanajeshi akibebelea silaha ya kivita wakati wa maandamano ya raia wanaopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza, Bujumbura, Mei 15 mwaka 2015. REUTERS/Goran Tomasevic
Matangazo ya kibiashara

Mashambulizi haya yalitiokea usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu Juni 22.

Mashambulio haya yanatokea siku moja baada ya mashambulizi mengine yaliyoendeshwa usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi juni 20 katika wilaya mbalimbali za mji wa Bujumbura. Mashambulizi ambayo yalilenga vituo vya askari polisi.

Askari polisi zaidi ya kumi na mmoja walijeruhiwa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo polisi iliwatuhumu waandamanji kuhusika na mashambulizi hayo, tuhuma ambazo waandamanaji walitupilia mbali.

Hali ya hofu imeendelea kutanda katika mji wa Bujumbura, huku kila upande ukiutuhumu mwengine kuhusika na mdororo wa usalama unaoshuhudiwa wakati huu nchini Burundi.

Wiki iliyopita chama tawala kupitia msemaji wake, Gelase Daniel Ndabirabe alisema akisisitiza kuwa upinzani na mashirika ya kiraia wamekua wakijiandaa kuendesha mashambulizi nchini Burundi wakitokea nchini Rwanda.

Wakati huo huo jeshi na polisi vilikanusha kuwa hakuna ishara za vita nchini Burundi, na kwamba hali ya usalama ni shwari kwa asilimia 100.

Kwa upande wao upinzani na vyama vya kiraia vimeendelea kuinyooshea kidole cha lawama serikali, hasa kundi la baadhi ya maafisa wa jeshi na polisi kutoka kundi la zamani la waasi la Cndd-Fdd, kwamba limekua likiandaa mpango wa kuwaangamiza watu wote wanaopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Hali hii inatokea wakati ikisalia wiki moja kulingana na tarehe iliyopangwa na rais Nkurunziza ili kufanyike uchaguzi wa wabunge na madiwani. Tarehe ambayo imetupiliwa mbali na upinzani wakibaini kwamba tarehe hiyo ilipangwa na upande mmoja bila makubaliano ya pande zote husika katika mchakato wa uchaguzi.

Hayo yakijiri raia wameendelea kuitoroka nchi. Mwishoni mwa juma hili lililopita mamia ya watu walivuka mpaka na kukimbilia nchi jirani za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania, kwa mujibu wa vyanzo vya Idara ya uhamiaji nchini Burundi, PAFE.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.