Pata taarifa kuu
BURUNDI-UN-AU-ICGLR-EAC-USALAMA-SIASA

Tume ya kimataifa ya usuluhishi yatoa wito kwa mazungumzo

Katika tangazo lililotumwa kwa RFI, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Ibrahima Fall, ametoa wito kwa wadau wote wanaohusika katika mgogoro wa Burundi, ikiwemo serikali, kuanza haraka mazungumzo, tangu Jumanne Juni 23, " katika masharti yaliyotolewa na Umoja wa Afrika ".

Polisi na waandamanaji uso kwa uso, wilayani Musaga, kusini mwa Bujumbura, Mei 4 mwaka 2015.
Polisi na waandamanaji uso kwa uso, wilayani Musaga, kusini mwa Bujumbura, Mei 4 mwaka 2015. RFI/SR
Matangazo ya kibiashara

Timu ya usulihishi wa kimataifa imekutana Jumatatu wiki hii kwa mara ya kwanza mjini Bujumbura. Timu hii inaundwa na Ibrahima Fall kutoka Umoja wa Afrika, Abdoulaye Bathily kutoka Umoja wa Mataifa, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Richard Sezibera pamoja na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR ), Profesa Ntumba Luaba, tangazo hilo limeeleza.

Wito huu unakuja wakati ambapo hali ya usalama nchini Burundi, hususan katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura imeendelea kudorora.

Watu zaidi ya wanne waliuawa na wengine zaidi ya ishirini walijeruhiwa katika mashambulizi ya guruneti dhidi ya baadhi ya baa za mikoa ya Kirundo, Ngozi na Kayanza, Kaskazini mwa Burundi.

Mashambulizi haya yalitiokea usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu Juni 22.

Mashambulio haya yalitokea siku moja baada ya mashambulizi mengine yaliyoendeshwa usiku wa Ijumaa kuamkia Jumamosi juni 20 katika wilaya mbalimbali za mji wa Bujumbura. Mashambulizi ambayo yalilenga vituo vya askari polisi.

Askari polisi zaidi ya kumi na mmoja walijeruhiwa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo polisi iliwatuhumu waandamanji kuhusika na mashambulizi hayo, tuhuma ambazo waandamanaji walitupilia mbali.

Hali ya hofu imeendelea kutanda katika mji wa Bujumbura, huku kila upande ukiutuhumu mwengine kuhusika na mdororo wa usalama unaoshuhudiwa wakati huu nchini Burundi.

Wiki iliyopita chama tawala kupitia msemaji wake, Gelase Daniel Ndabirabe alisema akisisitiza kuwa upinzani na mashirika ya kiraia wamekua wakijiandaa kuendesha mashambulizi nchini Burundi wakitokea nchini Rwanda.

Wakati huo huo jeshi na polisi vilikanusha kuwa hakuna ishara za vita nchini Burundi, na kwamba hali ya usalama ni shwari kwa asilimia 100.

Kwa upande wao upinzani na vyama vya kiraia vimeendelea kuinyooshea kidole cha lawama serikali, hasa kundi la baadhi ya maafisa wa jeshi na polisi kutoka kundi la zamani la waasi la Cndd-Fdd, kwamba limekua likiandaa mpango wa kuwaangamiza watu wote wanaopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Hali hii inatokea wakati ikisalia wiki moja kulingana na tarehe iliyopangwa na rais Nkurunziza ili kufanyike uchaguzi wa wabunge na madiwani. Tarehe ambayo imetupiliwa mbali na upinzani wakibaini kwamba tarehe hiyo ilipangwa na upande mmoja bila makubaliano ya pande zote husika katika mchakato wa uchaguzi.

Hayo yakijiri raia wameendelea kuitoroka nchi. Mwishoni mwa juma hili lililopita mamia ya watu walivuka mpaka na kukimbilia nchi jirani za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania, kwa mujibu wa vyanzo vya Idara ya uhamiaji nchini Burundi, PAFE.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.