Pata taarifa kuu
AU-BURUNDI-USALAMA-SIASA

AU yaamua kutuma haraka wataalam wa kijeshi Burundi

Umoja wa Afrika umeendelea kutiwa wasiwasi na hali ya kisiasa na usalama nchini Burundi, baada ya mazungumzo ya kisiasa kusimama ghafla, huku mpatanishi wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Burundi, Said Djinnit akijiuzulu kufuatia ombi la vyama vikuu 17 vya upinzani na mashirika ya kiraia yanayopinga muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Hali ya hofu imeendelea kutanda mjini Bujumbura, Burundi.
Hali ya hofu imeendelea kutanda mjini Bujumbura, Burundi. REUTERS/Goran Tomasevic
Matangazo ya kibiashara

Katika mkutano wa kilele wa 25 wa Umoja wa Afrika (AU) jijini Johannesburg Jumapili Juni 14, Umoja huo umeamuaa " kupelekwa haraka timu ya waangalizi wa Haki za Binadamu na wataalamu wa kijeshi kutoka Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya watakaosimamia mchakato wa kuwapokonya silaha wanamgambo pamoja na makundi mengine yenye silaha nchini Burundi ", Smail Chergui, Kamishna wa Amani na Usalama, ametangaza Jumatatu Juni 15.

Hayo yanajiri wakati ujumbe wa jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki umewasili tangu Jumapili usiku mjini Bujumbura. Ujumbe huo unaoundwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekutana Jumatatu wiki hii na rais Pierre Nkurunziza na vyama vikuu vya upinzani.

Mpaka sasa serikali ya Burundi bado inashikilia msimamo wake wa kufanyika kwa uchaguzi mkuu kulingana na kalenda mpya ya uchaguzi iliyotangazwa hivi karibuni.

Rais Pierre Nkurunziza kwa upande wake, kupitia tangazo lililotolewa na Ikulu ya rais Jumatatu mchana wiki hii, amesema kalenda haiwezi kamwe kubadilishwa, itasalia ile iliyopangwa hivi karibuni, ambapo inabaini kwamba uchaguzi wa wabunge na madiwani umepangwa kufanyika Juni 29, ule wa urais umepangwa kufanyika Jualai 15 na uchaguzi wa maseneta Julai 24.

Kuhusu timu ya wataalam wa kijeshi ambao watasimamia mchakato wa kuwapokonya silaha wanamgambo na makundi yenye silaha, rais Nkurunziza amebaini kwamba timu hiyo haina nafasi, kwani kuna kikosi kilichoteuliwa ambacho kimeanzisha zoezi hilo.

Marais zaidi ya hamsini walihuzuria mkutano huo wa 25 wa Umoja wa Afrika uliyofanyika mwishoni mwa juma lililopita, ambapo walitoa mapendekezo kadhaa ili kufanikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira mazuri nchini Burundi.

Mambo muhimu katika maazimio hayo yanapatikana katika Ibara ya 10 ya tangazo la Baraza la Amani na Usalama. Maamuzi sita yanatoa mwelekeo wa jinsi mambo yanavyopaswakwenda nchini Burundi. Jambo la kwanza ni kuanza kwa mazungumzo kati ya serikali ya Burundi na upinzani ndani ya wiki moja baada ya tangazo la baraza la Amani na Usalama, yaani Jumamosi ijayo.

Timu itakayosimamia mazungumzo itaundwa baada ya mazungumzo yatakayoendeshwa na uongozi wa Tume ya Umoja wa Afrika, chni ya mwamvuli wa rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la mjadala huu ni kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya uchaguzi, lakini pia kutatua masuala yote yanayosababisha mgongano kati ya pande husika nchini Burundi.

Uamzi wa tatu unahusu uchaguzi: kalenda iliyotangazwa na serikali, haitazingatiwa. Tarehe ya uchaguzi itawekwa kwa makubaliano ya pande zote husika katika mchakato wa uchaguzi kulingana na uamzi uliyochukuliwa na jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuahirisha uchaguzi kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu.

Baraza la amani na usalama pia limetangaza kutumwa aina tatu ya timu zake za wajumbe nchini Burundi. Timu ya kwanza itaundwa na waangalizi wa haki za binadamu, timu ya pili itajihusisha na kuchunguza mchakato wa kuwapokonya silaha wanamgambo, ambayo itaundwa na wataalam na wanajeshi. Na timu ya tatu itajielekeza Burundi kama masharti yatakua yameheshimishwa kwa ajili ya uchaguzi usiyokuwa na kasoro. Timu hii ni ya ujumbe wa waangakizi wa uchaguzi ambao utapelekea Umoja wa Afrika kuamua au la kutambua matokeo ya uchaguzi.

Na kuhakikisha utekelezaji wa maamuzi haya, ujumbe wa mawaziri kwa ushirikiano wa Tume ya Umoja wa Afrika utajielekeza wiki ya kwanza ya mwezi Julai nchini Burundi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.