Pata taarifa kuu
DRC-MACHAFUKO-UCHAGUZI-USALAMA-SIASA

Hali ya wasiwasi yaendelea kutanda Kinshasa

Hali ya machafuko imeendelea kwa siku ya tatu Jumatano Januari 21 katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kinshasa.

Maandamano dhidi ya kupitishwa sheria mpya ya uchaguzi, katika mji wa Kinshasa, Januari 19 mwaka 2015.
Maandamano dhidi ya kupitishwa sheria mpya ya uchaguzi, katika mji wa Kinshasa, Januari 19 mwaka 2015. AFP PHOTO/ PAPY MULONGO
Matangazo ya kibiashara

Polisi iliingilia kati kwa kuwatawanya kwa mara nyingine tena vijana ambao wanaonekana kumpinga rais wa nchi hyio Joseph Kabila.

Jumatano alaasiri, hali ya utulivu ilirejea katika mitaa mbalimbali ya mji wa Kinshasa, lakini bado hali ya wasiwasi imeendelea kutanda katika maeneo mbalimbali ya mji huo, hususan katika mabweni ya chuo kikuu cha Kinshasa.

Baada ya masaa kadhaa ya utulivu Jumatano alaasiri, hali ya wasiwasi imeendelea kutanda katika chuo kikuu cha Kinshasa, baada tu ya kuondoka katika chuo hicho Waziri mkuu Matata Ponyo, ambae ni afisa wa kwanza wa serikali kutembelea chuo kikuu cha Kinshasa tangu kuanza kwa machafuko hayo Jumatatu Januari 19 mwaka 2015.

Waziri Mkuu Matata Ponyo alipokewa na wanafunzi wenye hasira ambao walikua wakirusha mawe. Tangu hapo, hali ya wasiwasi imeendelea kushuhudiwa katika chuo kikuu hicho cha Kinshasa.

Kikosi cha usalama wa taifa kiliendelea kupiga doria katika mabweni ya chuo kikuu cha Kinshasa hadi jana jioni, huku kikiondoa vizuizi viliyowekwa na wanafunzi wa chuo kikuu hicho, bila hata hivyo kutokea kwa machafuko mapya.

Kwingineko ambako hali ya wasiwasi imeendelea kutanda ni katika hospitali kuu ya Kinshasa, ambapo wanajeshi wawili waliingia jana Jumatano alaasiri na kuanza kufyatua risasi hovyo. Watu watatu walijeruhiwa kwa risasi hizo, kwa mujibu wa chanzo cha hospitali.

Wakati huohuo Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo umetolea wito viongozi na upinzani kuheshimu Katiba na kujiepusha na vurugu.

Kanisa Katoliki, limetoa pia wito kufuatia machafuko hayo yanayoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Askofu mkuu wa Kinshasa, Laurent Monsengwo ametolea wito viongozi wa Congo kutowaua wananchi wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa viongozi, watu kumi na mmoja, akiwemo askari polisi na mwizi, wameuawa tangu Jumatatu Januari 19. Lakini shirika moja la haki za binadamu nchini Congo limebaini kwamba watu 28 ndio wameuawa mpaka sasa mjini Kinshasa.

Marekani ilizitolea wito hivi karibuni pande zote husika kusitisha vurugu, huku ikiomba uchaguzi ufanyike kulingana na jinsi “ Katiba” inavyoeleza.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.