Pata taarifa kuu
DRC

Jeshi la DRC lawasaka waasi wa M 23 milimani

Jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limeendelea kusonga mbele katika ngome za M 23 Mashariki mwa nchi hiyo wakati huu waasi hao wakijificha katika eneo dogo katibu na mpaka wa Rwanda.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatano, jeshi la FARDC likisaidiwa na lile la Umoja wa Mataifa limeendelea kupambana na waasi hao ambao wengine wao wamejificha katika milima ya Mbuzi Kilomita tatu kutoka mji wa Ntamugenga.

Jeshi la DRC linasema kuwa lengo la Oparesheni hiyo ni kuwasaka waasi wa M 23  ambao wamekujikusanya katika milima ya Runyonyi katibu na mpaka wa Uganda.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa MONUSCO  katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin Kobler mapema juma hili aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa kundi la waasi la M 23 sio tishio tena kijeshi Mashariki mwa nchi hiyo.

Kobler alieleza kuwa waasi wa M 23 wametoroka katika kambi zao za kijeshi na sasa wanajificha karibu na mpaka wa Rwanda baada ya kulemewa na wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakisaidiwa na wale wa Umoja wa Mataifa.

Mapigano kati ya waasi na majeshi ya serikali yalianza wiki iliyopita baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika jijini Kampala Uganda na kufikia siku ya Jumatatu jeshi la serikali lilifanikiwa kuchukua miji ya Rutshuru, Kiwanja na Rumangambo yote ambayo hapo awali ilikuwa inathibitiwa na waasi hao kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kurudishwa nyumba kwa waasi hao kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC ni ishara tosha waasi hao wamedhoofishwa kijeshi na huenda huu ndio ukawa mwisho wao.

Hata hivyo, waasi hao wa M 23 wanasema kuwa wamejiondoa katika ngome zao kwa muda tu ili kuuonesha ulimwengu kuwa wao hawataki vita kwa mujibu wa rais wa kundi hilo Betrand Bissimwa.

Wakaazi wa miji ya Rumangabo, Kiwanja, Rutshurum Buhumba na Kibumba wamekuwa wakisherehekea ushindi wa jeshi la serikali tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wachambuzi wa maswala ya migogoro wanasema utumizi wa nguvu za kijeshi sio suluhu ya kumaliza machafuko  Mashariki mwa DRC bali mazungumzo ya amani ndio yatakayomaliza machafuko hayo.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu 800,000 wamekimbia makwao baada ya kundi hilo la waasi kuanza Oparesheni zao Mashariki mwa nchi hiyo mwezi Aprili mwaka 2012.

Nchi za Rwanda na Uganda zimekanusha madai ya watalaam wa Umoja wa Mataifa kuwa wanawaunga mkono waasi hao wa M 23.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.