Rwanda yakana wanajeshi wake kukamatwa DRC wakiwasaidia waasi wa M 23
Serikali ya Rwanda imekanusha madai kuwa wanajeshi wake 20 walikamatwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kabla ya waasi wa M 23 kuuteka mji wa Goma mwezi uliopita.
Imechapishwa:
Msemaji wa jeshi la Rwanda Joseph Nzabamwita amesema tuhma hizo si za kweli na ikiwa wanajeshi hao wangekamatwa wangefikishwa mjini Goma, ambako kuna wanajeshi wengine wanaosaidia kulinda amani katika mpaka wake na DRC.
Serikali ya Kinshasa pamoja na wajumbe wa Umoja wa Mataifa wameendelea kuituhumu serikali ya Rwanda na Uganda kuwasaidia waasi wa M 23 kuuteka mji wa Goma, tuhma ambazo serikali za Kigali na Kampala zimekanusha.
Wakati hayo yakijiri, mazungumzo ya amani kati ya waasi wa M 23 na wajumbe wa serikali unaendelea kwa kusuasua jijini Kampala Uganda.
Kiongozi wa ujumbe wa serikali Waziri wa mambo ya nje Raymond Tshibanda amewatuhumu waasi hao kwa kutekeleza mauaji, ubakaji, wizi na kuwatesa raia wa Mashariki mwa nchi hiyo.
Aidha, serikali ya Kinshasa inasema ushahidi wa kutisha kuwa waasi hao wametekeleza visa hivyo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ushahidi ambao pia wanasema Jumuiya ya Kimataifa unao.
Naye mwakilishi wa waasi wa M 23 Francois Ruchogoza hakujibu tuhma hizo za serikali dhidi yao lakini hapo awali aliituhumu serikali ya Kinshasa kwa ubaguzi wa watu wenye asili ya Kinyarwanda Mashariki mwa nci hiyo.
Msuluhishi Mkuu wa mauzngumzo hayo ya amani Waziri wa Ulinzi Crispus Kiyonga, anasema ana matumaini ya kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda na suluhu litapatikana ili amani ipatikane Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.