Pata taarifa kuu
JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO-DRC

Rais wa DRC Joseph Kabila akiri uwepo wa mapungufu kwenye Uchaguzi Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC Joseph Kabila Kabange hatimaye kwa mara ya kwanza amejitokeza mbele ya wanahabari na kukiri uwepo wa mapungufu kwenye uchaguzi wa urais ambao umempa ushindi wa asilimia arobaini na tisa ya kura.

AFP/Gwenn Duborthomieu
Matangazo ya kibiashara

Rais Kabila ambaye amefanikiwa kutetea nafasi yake na kupata fursa ya kuendelea kukaa madarakani kwa miaka mitano mingine amesema kuwa hakubaliana na wale ambao wanasema uchaguzi huo si halali japokuwa hawezi kupinga suala la uwepo wa dosari.

Kiongozi huyo amewaambia wanahabari kuwa matokeo ya uchaguzi huo si batili kama ambavyo baadhi ya Taasisi za Waangalizi wa Kimataifa zilivyosema kwenye majumuisho yao lakini mapungufu yalikuwepo kama inavyokuwa kwenye chaguzi nyingine.

Rais Kabila bila ya kung'ata maneno alisema hadharani hakuridhishwa na taarifa ambayo ilitolewa na Kituo Cha Carter kuwa matokeo ya uchaguzi nchini humo ni batili kutokana na uwepo wa dosari chache ambazo zimeshuhudiwa.

Rais huyo ambaye anatarajiwa kuapishwa juma lijalo kuendelea na wadhifa wake amesema haikutosha kwa Kituo Cha Carter kusema uchaguzi huo si halali kwa kutembea vituo vya kuhesabia kura ishirini na tano kati ya mia moja sitini tisa vilivyokuwepo.

Akizungumzia suala la mpinzani wake Etienne Tshisekedi kujitangaza mshindi Rais Kabila amesema kuwa alishajitangaza kabla ya kupigwa kura, wakati wa zoezi la upigaji kura na hata kabla ya kumalizika kwa hesabu za kura.

Rais Kabila amesema hicho ni kitendo cha kawaida kwa wapinzani lakini kitu cha msingi ni kuheshimu matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi CENI ambayo yamempa ushindi yeye.

Kuhusu suala la kufanya uchunguzi wa vifo vilivyotokea wakati wa kusubiri matokeo ya mwisho ya urais kiongozi huyo amesema watasubiri ripoti kutoka polisi na kisha kuangalia nini ambacho kilichangia hali hiyo.

Naye Rais wa Tume Huru ya Uchaguzi CENI Daniel Ngoy amesema kuwa ripoti ambayo ilitolewa na Kituo Cha Carter haikuwa na ukweli wowote kwani imeshindwa kugusa maeneo yote na badala yake baadhi ya maeneo tu.

Huu ni uchaguzi wa pili wa kidemokrasia kufanyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC yangu kumalizika kwa machafuko yaliyosababisha umwagaji wa damu katika nchi hiyo na kufanikisha kuangushwa kwa Utawala wa Rais Mobutu Sese Seko.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.